Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano

(TCRA-CCC)

Haki za mtumiaji

Haki ya kupata huduma ya msingi

Mtumiaji wa huduma za mawasiliano ana haki ya kuhudumiwa kwa wakati na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Mtumiaji ana haki ya kupata huduma hizi kwa bei halali.

Haki ya Usalama

Mtumiaji ana haki ya kupata huduma salama kutoka kwa watoa huduma. Haki ya kulindwa dhidi ya bidhaa au huduma ambazo ni hatari kwa afya au maisha. Mtoa huduma anapaswa kujiridhisha kila wakati kuwa huduma anayopeleka kwa mtumiaji ni salama na haihatarishi usalama wa mtumiaji.

Haki ya kupata taarifa

Haki ya kupata taarifa sahihi na zinazotosheleza kuhusu huduma ili kumwezesha kufanya maamuzi sahihi na endelevu. Mtumiaji pia ana haki ya kupata taarifa juu ya sekta zinazosimamia mawasiliano nchini, juu ya sera, sheria na miongozo mbali mbali zinazoathiri huduma zinazotolewa kwa mtumiaji.

Haki ya kuchagua

Haki ya kuchagua huduma kwa kuzingatia bei, ubora, mahitaji na uwezo wa kifedha wa mtumiaji. Haki hii pia inategemea upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu huduma inayotolewa na watoa huduma.

Haki ya Kusikilizwa na Kuwakilishwa

Mtumiaji ana haki ya kuwakilishwa kwenye vyombo vya kutunga sheria, kusimamia sera ama kwa mdhibiti wa huduma za mawasiliano. Kuwakilishwa huku kunaenda sambamba na kupatiwa taarifa za masuala yaliyojiri yenye manufaa kwa mtumiaji.

Haki ya kufidiwa

Haki ya utatuzi mzuri wa madai, kufidiwa kutokana na kupatiwa bidhaa zenye dosari au huduma mbovu. Mteja anapaswa kukataa huduma zisizoridhisha na kurudishiwa fedha zake taslimu au kupatiwa bidhaa nyingine na mtoa huduma.

Haki ya Elimu

Mtumiaji ana haki ya kuelimishwa kuhusu huduma zinazotolewa ili kumpa maarifa na ujuzi kumwezesha kuchagua huduma stahiki. Mtumiaji ana haki ya kupata elimu na ujuzi unaohitajika kukufanya maamuzi ya msingi kwa kujiamini wakati wa kununua au kuchagua bidhaa au huduma. Haki ya kufahamishwa viwango, kanuni na taratibu za kitaifa na kimataifa zinazohusu mahitaji yake

Faragha

watoa huduma wana wajibu wa kuhakikisha na kudumisha usiri wa maudhui ya mawasiliano au data ambayo mtoa huduma anaweza kupata kutokana na kumhudumia mtumiaji. Taarifa za maudhui au data hazitatolewa kwa mtu yeyoye bila ridhaa ya mtumiaji au agizo la mamlaka na/au vyombo vya dola kulingana na sheria