News
TCRA CCC Yaendelea Kutoa Elimu ya Usalama Mtandaoni Nchini
Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano TCRA CCC kupitia Kamati zake za Mikoa, limeendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii nchini kuhusu matumizi salama na sahihi ya huduma za mawasiliano, haki na wajibu wa mtumiaji, pamoja na usalama wa watoto mtandaoni.
Katika Mkoa wa Manyara, Kamati ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano mkoani humo imetoa elimu kwa walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Darajani, iliyopo Kata ya Babati, Halmashauri ya Mji wa Babati.
Katika mafunzo hayo, wanafunzi wameelimishwa kuhusu usalama wa watoto mtandaoni, namna ya kujilinda na kuepuka hatari zinazoweza kujitokeza wanapotumia mitandao ya kijamii na intaneti kwa ujumla. Kwa upande wa walimu, elimu iliyotolewa ilijikita katika namna ya kulinda taarifa zao binafsi na umuhimu wa kuheshimu faragha ya watumiaji wengine. Jumla ya washiriki 253 wamenufaika na elimu hiyo, wakiwemo walimu 20 na wanafunzi 480.
Mkoani Tabora, Kamati ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Mkoa wa Tabora, tarehe 15 Oktoba 2026, imetoa elimu kwa wajasiriamali kutoka Kata ya Isevya, katika mafunzo yaliyofanyika katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Isevya.
Elimu hiyo imetolewa kufuatia kuwepo kwa wimbi la utapeli wa fedha kupitia mitandao, ambapo wajasiriamali hao wamewezeshwa namna ya kulinda taarifa zao binafsi, ikiwa ni pamoja na kutoamini na kumpa mtu yeyote nywila (password) zao au kifaa cha mawasiliano.
Aidha, wajasiriamali hao pia wameelimishwa kuhusu namna ya kuwalinda watoto dhidi ya matumizi holela ya mitandao na umuhimu wa kufuatilia mienendo ya watoto wao pindi wanapotumia mitandao.
Hata hivyo tarehe 17 Oktoba 2026, Kamati hiyo pia ilitoa elimu kwa wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Tabora, ambao ni walimu watarajiwa. Jumla ya washiriki 232 walinufaika na elimu hiyo, wakiwemo wanafunzi wa kike 140, wanafunzi wa kiume 90, mwalimu wa kike 1 na mwalimu wa kiume 1.
Katika mafunzo hayo, washiriki waliwezeshwa kuhusu haki na wajibu wa mtumiaji wa huduma za mawasiliano, utaratibu wa kuwasilisha malalamiko, Sheria ya Makosa ya Mtandao, aina za makosa ya mtandao na adhabu dhidi ya ukiukwaji wa sheria, pamoja na namna ya kuwasilisha hoja za mtumiaji kupitia Consumer Portal.
Wanafunzi na walimu hao walivutiwa na kufurahia mafunzo hayo, kwani mengi yaliyojadiliwa walikuwa hawajui kwa undani zaidi, na wameahidi kuwa mabalozi wa kufikisha elimu hiyo kwa wenzao ambao hawakupata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo.
Wakati huo huo, mkoani Iringa, Kamati ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Mkoa wa Iringa imeendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii mkoani humo kuhusu haki na wajibu wa mtumiaji wa huduma na bidhaa za mawasiliano pamoja na usalama wa watoto mtandaoni.
Mjumbe wa Kamati hiyo, Bw. Stephano Mwakipesile, Alielimisha waumini kwenye semina iliyofanyika Katika kanisa la TAG Kata ya Mwangata, Manispaa ya Iringa. Washarika hao walipatiwa elimu kuhusu haki na wajibu wao wanapotumia huduma na bidhaa za mawasiliano. Jumla ya washiriki 30 walihudhuria semina hiyo, wakiwemo wanawake 18 na wanaume 12.
Kamati hiyo pia ilitoa elimu kwa wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Mawelewele iliyopo Manispaa ya Iringa. Mada zilizotolewa ni usalama wa watoto mtandaoni, pamoja na haki na wajibu wa mtumiaji wa huduma na bidhaa za mawasiliano. Jumla ya washiriki 378 wamenufaika na elimu hiyo shuleni hapo, wakiwemo wanafunzi 364 (wasichana 234 na wavulana 130) na walimu 14
Elimu inayoendelea kutolewa na TCRA CCC kupitia Kamati zake za Mikoa ni sehemu ya juhudi za Baraza hilo kuongeza uelewa wa jamii kuhusu matumizi salama na sahihi ya huduma za mawasiliano, ili kuwalinda watumiaji dhidi ya utapeli na hatari nyingine za mtandaoni, sambamba na kuwajengea uwezo wa kutambua haki na wajibu wao.


