Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

TCRA Consumer Consultative Council (TCRA-CCC)

Corporate logo

Importance of Online Protection Education

UMUHIMU WA ELIMU YA USALAMA MTANDAO

Mambo Kumi (10) Unayoweza Kufanya

1. Jiridhishe kabla ya kufungua au kupakua chochote mtandaoni

Ikitokea umepokea barua pepe inayoonekana imetoka Kwa mtu unayemfahamu, kuwa makini kabla ya kufungua viambatisho vyake. Ni vema ukiwa na mashaka uchukue tahadhari au kutojibu barua pepe husika kwa sababu utambulisho wa mhusika unaweza kuwa umedukuliwa.

2. Tumia programu za kujilinda mtandaoni

Programu ya kulinda vifaa vya TEHAMA (AV) imekuwa suluhisho zuri la kupambana na mashambulizi ya virusi mtandaoni. Programu ya AV huzuia virusi vya mtandao kuingia kwenye kifaa chako na kuhatarisha usalama wa taarifa. Inashauriwa kutumia programu moja ya kuzuia virusi mtandaoni kutoka kwa wachuuzi wanaoaminika

3. Jiridhishe maombi ya taarifa binafsi

Unapoombwa kutoa taarifa zako binafsi au za mtu mwingine, hakikisha unajiridhisha na utambulisho wa mwombaji - hata kama inaonekana kuwa ni mtu unayemfahamu. Matapeli wana mbinu nyingi za kukusanya, kuiba taarifa au utambulisho wa mtu ili kuzitumia kufanya uhalifu. Jenga tabia ya kuangalia mara kwa mara taarifa zako za kifedha.

4. Linda nywila zako

Usitoe nywila au nambari ya siri (PIN) kwa mtu yeyote. Hakikisha nywila ni ndefu, imara na ya kipekee. inashauriwa utumie uthibitishaji wa vipengele vingi kadiri ya inavyowezekana (mfano alama za vidole, kadi, jumbe za uthibitisho kwa namba binafsi za simu au barua pepe, n.k.).

  • Tumia programu za kulinda nywila kama vile Last Pass au RoboForm;
  • Tumia nywila/nambari ya siri tofauti kwa akaunti tofauti;
  • Tumia nywila/nambari ya siri tofauti kazini na nyumbani; na
  • Usikubali programu na tovuti kukumbuka nywila zako.

5. Matumizi salama ya vifaa vya TEHAMA vya mkononi

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kampuni ya McAfee Labs ya Marekani, matukio mapya milioni 1.5 ya programu hasidi na virusi mtandaoni yanalenga zaidi vifaa vya TEHAMA vya mkononi.

Dondoo muhimu za usalama wa vifaa vya TEHAMA vya mkononi:

  • Tengeneza Nambari ya siri (PIN) ya kipekee. Inashauriwa kutotumia tarehe ya kuzaliwa au namba ya simu;
  • Sakinisha (Install) programu tumizi (Application) kutoka kwenye vyanzo vinavyoaminika;
  • Hakikisha kifaa chako kimesasishwa (updated) - Wadukuzi hutumia udhaifu uliopo katika programu au mifumo ambayo haijasasishwa kuingilia vifaa au

mifumo husika;

6. Linda vifaa vyako vya kielektroniki

Kuwa makini na vifaa vyako vya kielektroniki unapokuwa katika maeneo ya umma. Hakikisha unafunga vifaa vyako au uende navyo, hata kama utatoka kwa sekunde chache. Ukiwa kazini, chukua tahadhari ya eneo lako na ufunge skrini ya kompyuta yako kabla ya kutoka kwenye meza yako. Jenga tamaduni ya kuchukua simu yako na vifaa vingine vinavyobebeka.

7. Sasisha vifaa vyako, vivinjari (browsers) na programu

Sasisha vifaa vya TEHAMA, vivinjari na programu mara kwa mara ili kupunguza mianya ya udukuzi na wahalifu wa mtandao kuingilia programu au vifaa husika.

8. Hifadhi nakala za faili muhimu

Hifadhi nakala katika maeneo tofauti (physical location) na uzifungue mara kwa mara. Kwa faili muhimu za kazi, nakala rudufu zihifadhiwe kwenye hifadhi tofauti (mfano wingu kompyuta au USB iliyosimbwa (encrypted)) ili kuihifadhi kwa usalama.

9. Usitumie Wi-Fi ya bure (Public Wi-Fi)

Inashauriwa usitumie Wi-Fi ya bure isiyohitaji kuingiza nywila bila kutumia programu ya Mtandao Pepe wa Kibinafsi (VPN). Kwa kutumia programu ya VPN, taarifa kati ya kifaa chako na seva ya VPN imesimbwa kwa njia za kitaalamu.

Hii inamaanisha kuwa ni vigumu zaidi kwa mhalifu wa mtandao kuzifikia taarifa zako kwenye kifaa husika. Inashauriwa kutumia mtandao wa mtoa huduma wa simu endapo hauna VPN ili kuwa salama.

10. Ukiwa na mashaka, toa taarifa!

Jifunze jinsi ya kutambua viashiria vya uhalifu kimtandao ambavyo vinaleta mashaka. Ripoti masuala yote ya kihalifu mtandao kwenye Kituo cha Polisi kilicho karibu nawe