News
Kampeni Dhidi ya Utapeli Mtandaoni Yaendelea Kushika Kasi
Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA CCC) kupitia Kamati ya Watumiaji Mkoa wa Iringa limeendelea kutoa elimu ya utapeli mtandaoni kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Isakaliko ikiwa ni sehemu ya kampeni maalumu ya "Sitapeliki" ili kuwalinda na changamoto za mtandaoni katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Kampeni hii ilizinduliwa rasmi tarehe 20, Februari 2025 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb), jijini Arusha. Lengo ni kuwaelimisha watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini kuhusu utapeli mtandaoni na kuwapa tahadhari na namna bora ya kujilinda mtandaoni.
Katika Mkoa wa Iringa, kampeni hii ya “Sitapeliki” imeendelea kutolewa na Kamati ya Watumiaji Mkoa wa Iringa kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Isakaliko iliyopo kata ya Kitasengwa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na kuweza kuwafikia jumla ya wanafunzi 234 (Wavulana 130, wasichana 104) pamoja na walimu 13.
Aidha; Kamati imetoa elimu juu ya umuhimu wa kutumia nywila imara, kuhakikisha Watumiaji wanawasiliana na mtoa huduma kwa kupiga namba 100 pekee na endapo watakutana na ujumbe wa kitapeli, wanapaswa kuripoti kwa kutuma ujumbe waliotumiwa kwenda namba 15040, kuhakiki usajili wa laini zao kwa kupiga *106# na kuepuka kubofya viunganishi (links) wasivyokuwa na uhakika navyo ili kuepuka kutapeliwa kwa njia ya mtandao.
Katika muktadha huo huo, Katibu wa Kamati ya Watumiaji Mkoa wa Iringa Ndg. Edina Byemerwa amesema kuwa, “wanafunzi wanapaswa kuwa makini wanapokuwa mtandaoni ili kujilinda dhidi ya watu wenye nia ovu kama mafataki, wadhalilishaji na matapeli.”
Kwa pamoja, tunaweza kuifanya mitandao kuwa mahali salama kwa kila mtumiaji wa mawasiliano nchini.
#SITAPELIKI
#KuwaSmart
#HudumaBoraYaMawasilianoNiHakiYako