News
Wananchi Watakiwa Kufahamu Haki na Wajibu Wao
Tabora na Mbeya
Wananchi wametakiwa kufahamu haki na wajibu wao wanapotumia huduma mbalimbali za mawasiliano ili kuepuka changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza.
Akitoa elimu kwa wananchi wa Sikonge mkoani Tabora katika Siku ya Wanawake Duniani 2026, Katibu wa Kamati ya Watumiaji Mkoa wa Tabora, ndugu Joachim Milambo amesema kutojua wajibu humfanya mtumiaji kuona ana haki ya kutumia simu vyovyote apendavyo.
"Usipojua haki zako, hata mtu asiye na nia njema anapofanya jambo lililo kinyume na utaratibu, utashindwa kujua ni hatua gani za kuchukua!", amesema Milambo.
Wakati hayo yakijiri Tabora, mkoani Mbeya Kamati ya Watumiaji Mkoa wa Mbeya imeshiriki Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa kuzungumza na wajasiriamali kuhusu fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya mawasiliano endapo wataitumia sekta hiyo kwa tija.
Mwenyekiti wa Kamati ya Watumiaji Mkoa wa Mbeya, Idd Mwalukali amesema simu ni ofisi na chanzo kizuri cha mapato kikitumika vizuri.
Aidha; Mwalukali amewasihi wananchi kuacha tabia ya kuwaamini ndugu, jamaa na marafiki kwa kuwapa nywila za simu zako kwani ni hatari kwa usalama wa taarifa zao.
Machi 8 ya kila mwaka, ni Siku ya Wanawake duniani ambayo kwa Tanzania mwaka 2026, Maadhimisho yamebebwa na kaulimbiu isemayo Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050.


