Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano

(TCRA-CCC)

Maswali Yaulizwayo Mara kwa Mara

TCRA CCC ni nini?

TCRA CCC au Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano ni taasisi ya umma iliyoundwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano ya mwaka 2003 kwa lengo la kulinda na kutetea maslahi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano.

TCRA CCC inalindaje na kutetea haki na maslahi ya watumiaji?

Kutetea na kulinda maslahi ya watumiaji kwa kuwasilisha maoni na taarifa pamoja na kushauriana na Mamlaka, na Waziri mwenye dhamana ya mawasiliano,kupokea na kusambaza taarifa kuhusu maslahi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano, kuanzisha kamati za watumiaji wa huduma za mawasiliano za mikoa pamoja na kushauriana nazo; kushauriana na watoa huduma, Serikali na vikundi vingine vya watumiaji juu ya masuala yanayohusu watumiaji.

Haki za mtumiaji ni zipi?

Mtumiaji ana haki ya kupata huduma za mawasiliano; haki ya kuchagua huduma, haki ya kupata huduma na bidhaa zenye ubora, haki ya kupata elimu, haki ya kusikilizwa, haki ya kulalamika, haki ya kupata taarifa na haki ya kupata usiri/faragha

Mtumiaji ana wajibu gani?

Mtumiaji ana wajibu wa kulipia gharama za huduma anazotumia, kutafuta taarifa, kutunza mazingira, kulalamika, kulinda miundo mbinu ya mawasiliano pamoja na kuhakikisha kuwa anatumia huduma na bidhaa za mawasiliano kwa usahihi kulindana na kanuni na sheria zilizopo.

Ni mambo gani yanaweza kulalamikiwa na mtumiaji?

Mtumiaji anaweza kulalamika kuhusu:

  • Kutopatikana kwa huduma
  • Huduma zisizokidhi viwango
  • Ukiukwaji wa usiri au faragha
  • Kukatiwa huduma bila sababu za msingi
  • Bidhaa isiyokidhi viwango
  • Matangazo ya biashara yenye udanganyifu n.k

Ni utaratibu gani mtumiaji atafuata kuwasilisha malalamiko?

Mtumiaji asipopata haki zake ana haki ya kulalamika kwa kufuata utaratibu uliowekwa kisheria. Utaratibu huu unamtaka mtumiaji kuwasilisha malalamiko yake kwa mtoa huduma, endapo tatizo halijapata utatuzi mtumiaji atawasilisha malalamiko yake kwa maandishi kwa Mamlaka ya Mawasiliano yaani TCRA.

Mtumiaji anashauriwa pia kutuma nakala kwa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano.