News
Online Fraud Education Continues in Ruvuma Region
Ruvuma.
Katika kampeni maalumu ya "SITAPELIKI" dhidi ya utapeli mtandaoni nchini, Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA CCC) kupitia Kamati ya Watumiaji Mkoa wa Ruvuma limeendelea kutoa elimu ya utapeli mtandaoni ili kuwalinda watumiaji wa huduma za mawasiliano na wananchi kwa ujumla dhidi ya hasara zinazotokana na ulaghai mtandaoni. Machi 18, 2025.
Kampeni hii ilizinduliwa rasmi tarehe 20, Februari 2025 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb), jijini Arusha. Lengo ni kuwaelimisha watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini kuhusu mbinu za walaghai wa mtandaoni na kuwapa tahadhari kuhusu namna bora ya kujilinda.
Katika Mkoa wa Ruvuma, kampeni hii ya “Sitapeliki” imeendelea kutolewa na Kamati ya Watumiaji Mkoa wa Ruvuma katika sehemu mbalimbali ili kuwasaidia Watumiaji waweze kujilinda dhidi ya utapeli mtandaoni na wiki hii Kamati imewatembelea wanafunzi wa Shule ya Sekondari Matarawe, Manispaa ya Songea.
Aidha, Kamati ya Watumiaji Mkoa wa Ruvuma imeweza kuwafikia takribani wanafunzi 800 wa shule hiyo na Wazazi wapatao 300 waliokuwepo katika shule hiyo wakati wa kikao cha wazazi kilicho jadili mambo mbalimbali yakiwemo ya ufaulu, nidhamu kwa watoto pamoja na ukaribu wa wazazi kwa watoto wao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Watumiaji Mkoa wa Ruvuma Ndg. Judith Erasto Mbogoro amesema kuwa, watumiaji wana haki ya kujua namna ya kujilinda kwa kufuata taratibu mbalimbali kama; kuwa na nywilla (Password) imara, kuwasiliana na mtoa huduma kupitia namba 100 pekee, kutoa taarifa za utapeli kwa kutuma ujumbe kwenda namba 15040, kuhakiki usajili wa laini kwa kupiga *106#, kuepuka kubofya viunganishi (links) visivyo julikana na kutokutoa taarifa binafsi kwa mtu mwingine bila kujiridhisha.
Utapeli wa mtandaoni unaendelea kuathiri watumiaji wengi nchini na kampeni hii inalenga kuwapa wananchi maarifa sahihi ya kujilinda dhidi ya matapel na ili kusaidia mapambano haya, wananchi wanahimizwa kuripoti matukio ya utapeli kwa kutuma ujumbe mfupi wa taarifa za utapeli kwenda namba 15040.
Kwa pamoja, tunaweza kuifanya mitandao kuwa mahali salama kwa kila mtumiaji wa mawasiliano nchini.
*#SITAPELIKI*
*#KuwaSmart*
*#HudumaBoraYaMawasilianoNiHakiYako*