News
Ulinzi wa Mtoto Mtandaoni ni Kipaumbele Chetu - TCRA CCC
Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Mawasiliano nchini TCRA CCC limesema kuwa Ulinzi na Usalama wa Mtoto wa Kitanzania ni kipaumbele kisicho na mbadala.
Akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kashai iliyopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Mwenyekiti wa Kamati ya Watumiaji Mkoa wa Kagera, Prosper Mbakile, amewataka wanafunzi wa hao kuripoti mara moja kwa Walimu, Wazazi na Polisi wanapoona matukio ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
"TCRA CCC itaendelea kuhakikisha mnakuwa salama dhidi ya watu wenye nia ovu kwenye mawasiliano," amesema Prosper Mbakile, Mwenyekiti wa Kamati ya Watumiaji Mkoa wa Kagera.
Jumla ya wanafunzi 1604 wa Shule hiyo walipata Elimu kuhusu Ulinzi na Usalama wa Mtoto mtandaoni.
Nako mkoani Kigoma, TCRA CCC kwa kushirikiana na Kamati ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano mkoani humo imetoa Elimu kwa Wanafunzi wa Shule ya Msingi Bangwe juu ya madhara ya matumizi mabaya ya mitandao hasa kwa watoto.
Kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la UNICEF wa mwaka 2022 kwa watoto wa Tanzania wenye umri wa miaka 12 hadi 17 ulioonesha asilimia 67 ya watoto wanatumia mitandao na asilimia 4 ya watoto hao walifanyiwa aina tofauti za ukatili kwenye mitandao ikiwa pamoja na kukutana na wahalifu waliowasiliana nao kupitia mitandao.