News
TCRA CCC: Wazazi Lindeni Watoto Mtandaoni
Wazazi na Walezi nchini wametakiwa kuwa walinzi wa kwanza kwa Watoto wao katika mitandao ya Kijamii ili kuepusha madhara yoyote yanayoweza kuwakabili watoto.
Wakitoa Elimu kwa Wazazi na Walezi waliojitokeza kwenye Mahafali ya Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Ibumu mkoani Iringa, Kamati ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano mkoani humo imesema Watoto wanahitaji uangalizi wa Wazazi ili wasipotoke.
"Haiwezekani Mzazi unamnunulia simu Mtoto halafu hufuatilii anaitumia vipi. Kaingia Mtandaoni hujui anachati nini na anachati na nani! Wewe ndio Mlinzi wa kwanza wa Mtoto!" Amesema Mwenyekiti wa Kamati ya Watumiaji mkoani Iringa Raphael Mtitu.
Kamati hiyo ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Iringa imetembelea pia Shule ya Msingi Kigamboni na Shule ya Msingi Ilala zote za Manispaa ya Iringa mkoani Iringa.
TCRA CCC imeendelea na Kampeni yake ya kuimarisha Ulinzi wa Mtoto Mtandaoni na kukuza uelewa kuhusu Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ili kuhakikisha dhamira ya serikali ya Uchumi imara na salama wa kidijitali unafikiwa.


