Online Child Protection
Endapo watoto watatumia mitandao bila usimamizi wa wazazi au walezi wanaweza kukutana na changamoto zifuatazo;
- Kuwasiliana na watu wasiofaa.
- Wahalifu mtandaoni: ambao hutumia njia za ulaghai kuwashawishi watoto kutoa taarifa nyeti kuhusu wao wenyewe au wazazi wao
- Wanyanyasaji wa mtandaoni (Cyber bullies): ambao mara nyingi huwa na malengo ya kuwanyanyasa watoto kisaikolojia na kuwasababishia hofu au msongo wa mawazo.
- Mafataki wa mtandaoni (Online Sexual Predators): ambao malengo yao ni kuwarubuni Watoto kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi.
- Kukumbana na maudhui yasiyofaa kama vile:
- Maudhui ya ngono na picha za utupu.
- Matukio ya kihalifu na biashara haramu.
- Habari potofu.
- Kupakua programu hatarishi au virusi vya kompyuta (malware) kupitia tovuti hatarishi, kubofya viunganishi hatarishi na pia kufungua viambatisho vya barua-pepe vyenye virusi vya kompyuta, na hivyo kusababisha uharibifu wa taarifa na vifaa vya kielektroni.
- Matumizi ya kupindukia (Addiction): Fursa mbalimbali zinazopatikana mtandaoni kama vile michezo ya kompyuta, mitandao ya kijamii, katuni na muziki huwavutia sana watoto ambapo baada ya muda huwafanya watoto kuwa watumwa wa mtandao.
- Changamoto hizi zinaweza kupelekea kushuka kwa maendeleo ya watoto kitaaluma na kupata athari nyingine za kisaikolojia kama vile kuwa na msongo wa mawazo n.k
Angalizo kwa Watoto
- Usitumie mitandao bila idhini ya wazazi au walezi.
- Epuka kuwasiliana na watu usiowafahamu mtandaoni.
- Usichapishe taarifa binafsi kuhusu wewe, mzazi au mlezi wako kama vile tarehe ya kuzaliwa, anwani ya makazi, nywila (password).
- Epuka kutoa au kuchapisha taarifa hatarishi kama vile picha au video za utupu, vurugu au vitisho.
- Usichapishe chochote kuhusu watu wengine bila ridhaa yao.
- Elewa mipangilio na usome mikataba ya faragha kabla ya kutumia programu yoyote mtandaoni. Vinginevyo, unaweza kuruhusu taarifa zako kuingiliwa au kuonwa na watu wengine pasipo wewe kujua.
- Zuia (block) mtu yeyote anayetuma maoni ya kukusumbua, kukutishia au yasiyofaa kuhusu wewe na kuripoti kwa mtoa huduma wa programu husika au kituo cha Polisi karibu nawe.
- Chagua nywila (password) salama yenye tarakimu nane hadi kumi na mbili zenye mchanganyiko wa herufi, nambari na herufi za alama mfano “D0nt4g@t!” na uibadilishe mara kwa mara, angalau kila baada ya miezi mitatu (3).
- Kumbuka nywila (password) ni siri yako. Tumia programu za kujikinga na virusi vya kompyuta na hakikisha programu hiyo inahuishwa mara kwa mara.
Mzazi fanya yafuatayo kumlinda mwanao mtandaoni;
- Muhamasishe Mtoto kutumia mitandao ili umsaidie kwenye masomo yake (kitaaluma Zaidi) na si vinginevyo.
- Jifunze kila kitu kwa mapana kuhusu mtandao. Kuzoea mtandao hakutakusaidia tu kuelewa athari, lakini pia kukusaidia kuzungumza na watoto wako.
- Weka mipaka ya mambo ambayo mtoto wako anaweza na ambayo hawezi kuyafanya mtandaoni. Ni muhimu kuweka masharti kwa mtoto wako ili ajue wajibu wake na mipaka yake pindi awapo mtandaoni. Usisubiri hadi kitu kibaya kitokee kwake.
- Weka udhibiti ikiwa ni pamoja na kuchuja maudhui yasiyofaa kwa kutumia programu maalumu za kompyuta (parental control programs) kwenye vifaa vyako vya kompyuta.
- Mfundishe mtoto wako namna ya kulinda taarifa binafsi. Kwa kawaida siyo salama kuchapisha taarifa binafsi mtandaoni kama nambari za simu, anwani, nywila (password) na namba ya kadi ya benki. Ikiwa wahalifu wanapata taarifa hizi, wanaweza kuzitumia vibaya dhidi yake au familia yako.
- Zungumza na mtoto wako juu ya matumizi sahihi na salama ya mtandao ikiwemo mitandao ya kijamii ambayo huruhusu watumiaji wake kushiriki picha, video na majadiliano kati ya marafiki au wageni.
- Muhamasishe mtoto wako kutoa taarifa kwako endapo atakutana na tatizo lolote mtandaoni. Ikiwa mtoto wako anapata tatizo mtandaoni, mshauri aje kwako au awasiliane nasi kupitia tovuti yetu au namba za simu badala ya kuacha. Kumbuka kwamba upo uwezekano wa mtoto wako kukumbana na maudhui yasiyofaa au tukio hatarishi mtandaoni, hata kama wanafanya kila kitu kwa usahihi.