News
Consumer Rights Day to be held in Morogoro Region
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Dar es Salaam, Tanzania, 10 Machi 2025
Jukwaa la Watumiaji Tanzania (TCF) kwa kushirikiana na The Foundation for Civil Society (FCS), linawakaribisha wananchi wote kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Haki ya Mtumiaji Duniani ambayo kitaifa yatafanyika mjini Morogoro tarehe 15 Machi 2025. Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu ni ‘Haki na Maisha Endelevu kwa Mtumiaji’ ambapo lengo ni kuhamasisha walaji na wadau wa huduma zinazodhibitiwa nchini kubadilisha mitindo yao ya maisha kwa kuzingatia matumizi endelevu.
Siku hii muhimu huadhimishwa kimataifa ili kuhamasisha ulinzi wa haki za watumiaji na kukuza matumizi endelevu. Lengo ni kuelimisha umma kuhusu haki zao kama watumiaji na kuhimiza serikali, mashirika, na wadau mbalimbali kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha uwepo wa huduma bora, salama, na za haki kwa watumiaji katika sekta mbalimbali.
“Watumiaji wanapaswa kuzingatia matumizi salama na endelevu huku wakipewa nafasi katika kufanya maamuzi yanayohusu huduma wanazotumia. Ni haki yao kupata huduma bora, salama, na kwa gharama nafuu. Ni jukumu letu kutoa elimu hii kuhakikisha kuwa tunaelekea kwenye matumizi endelevu kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo,” alisema ndugu Daud Daud, Mwenyekiti wa TCF, ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa LATRA-CCC na kuongeza;
“Ili kufikisha ujumbe kwa watumiaji, wadau wa sekta zinazodhibitiwa nchini, na Watanzania kote nchini, tunakusudia kutumia vyombo vya habari zikiwemo redio, televisheni, na mitandao ya kijamii kufikisha elimu hii muhimu kwa jamii. Pia, tutakuwa na semina kwa asasi za kiraia mjini Morogoro siku ya kilele, tarehe 15 Machi 2025, ambapo mkazo utakuwa ni elimu kwa watumiaji kubadili mwelekeo kwa kutambua haki zao na kuzingatia matumizi endelevu”.
Tunasisitiza umuhimu wa matumizi salama na endelevu katika sekta za nishati, mawasiliano, na usafiri wa anga. TCF inatambua dhamira ya Serikali ya kufikia asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034, na hivyo tunatoa wito kwa watumiaji kupokea mabadiliko haya yenye lengo la kulinda afya zao pamoja na mazingira.
Usalama katika mawasiliano na matumizi ya mawasiliano mtandaoni, ikiwemo ulinzi wa faragha ya watumiaji ni jambo ambalo tunalipa uzito mkubwa. Tutatumia maadhimisho haya kuhimiza matumizi salama na endelevu katika enzi hizi za akili mnemba na uhalifu mtandaoni. Sambamba na hilo, tunasisitiza kuzingatia matumizi salama na endelevu katika usafiri wa anga na nchi kavu kwa manufaa ya watumiaji na ukuaji wa uchumi wa taifa kwa ujumla.
“Tunatoa wito kwa vyombo vya habari kuungana nasi katika kuhamasisha na kutoa elimu kwa watumiaji kote nchini kuhakikisha wanazingatia matumizi salama na endelevu, huku watoa huduma katika sekta zinazodhibitiwa wakizingatia utoaji wa huduma bora, salama na nafuu kwa wateja wao”, alimaliza Bw. Daud.
Maadhimisho ya Siku ya Haki ya Mtumiaji nchini Tanzania, huandaliwa na kuratibiwa na Jukwaa la Watumiaji Tanzania, linaloundwa na taasisi zinazowatetea watumiaji nchini, ambazo kwa mwaka huu zimejumuisha LATRA CCC, TCAA CCC, EWURA CCC, na TCRA CCC kwa kushirikiana na the Foundation for Civil Society (FCS).
MWISHO.