News
TCRA CCC: Wasaidieni Wananchi wajue Haki na Wajibu wao kwenye Huduma za Mawasiliano.
Singida
Kamati ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Mkoa wa Singida imewahimiza Wenyeviti wa serikali za mitaa Mkoa wa Singida kuwaelimisha wananchi wanaowaongoza kujua Haki na Wajibu wao pale wanapotumia huduma za mawasiliano.
Akizungumza na wenyeviti wa serikali za mitaa katika Manispaa ya Singida, Mwenyekiti wa Kamati ya Watumiaji Mkoa wa Singida Abdi Keira amesema mikutano wanayofanya wenyeviti wa serikali za mitaa ni jukwaa muhimu pia la kuwafikishia wananchi elimu hiyo.
"Mwingine anasajiliwa laini ya simu, anatoa mpaka nywila yake (Password), kumbe hajui kuwa anatapeliwa. Hawa wananchi mnaishi nao, waelimisheni."amesisitiza mwenyekiti wa kamati hiyo.
Pia Keira ambaye alimwakilisha Katibu Mtendaji wa TCRA CCC Bi Mary Shao Msuya, amesema wananchi wakijua Haki na Wajibu wao, hawatashiriki kusambaza ujumbe wa chuki, matusi na lugha zisizofaa kwa wengine.


