News
TCRA CCC Yateta na Wanafunzi wa Chuo cha King Rumanyika Kagera
Kamati ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Mkoa wa Kagera imewasihi wanafunzi wa vyuo nchini kuifahamu vyema Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 ili kujua Haki na Wajibu walio nao.
Akizungumza na Wanachuo wa Chuo cha King Rumanyika kilichopo katika Kata ya Nshambya mkoani Kagera, Mwenyekiti wa Kamati ya Watumiaji Mkoa huo ndugu Prosper Mbakile amesema Vijana kuijua Sheria hiyo kutawaepusha na makosa ya mtandaoni wanayotenda pasi na kujua.
"Unakuta Kijana amemtukana mwenzie kwenye mtandao kama vile Instagram au amemkashifu. miezi kadhaa imepita, kasahau, anashangaa kakamatwa, kumbe mwenzie alishtaki. Sasa, hivi ni vitu vidogo vidogo ambavyo unaweza kupuuza kumbe ni kosa la kimtandao! Jielimisheni Ndugu zangu!", amesema Mbakile.
Kamati hiyo ya Watumiaji Mkoa wa Kagera inaendelea na Kampeni ya kuelimisha makundi mbalimbali kuhusu matumizi sahihi ya Mawasiliano ikiwa ni Mkakati wa kuwafikia Watanzania Nchi nzima, unaoendeshwa na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano nchini (TCRA CCC) kama hatua mojawapo ya kusaidia watumiaji kufahamu Sheria na Miongozo mbalimbali ambayo inasimamiwa matumizi sahihi na salama ya huduma za mawasiliano.


