Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

TCRA Consumer Consultative Council (TCRA-CCC)

Corporate logo

News

TCRA CCC Yaendelea na Kampeni ya Elimu ya Matumizi Sahihi na Fursa Zilizoko Katika Sekta ya Mawasiliano Nchini


Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano nchini (TCRA CCC) kupitia Kamati za Watumiaji za Mikoa, limeendelea na zoezi la kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano na fursa zilizoko katika sekta ya mawasiliano. Maelfu ya watumiaji wamenufaika kupitia mikutano na maadhimisho mbalimbali yaliyofanyika mikoa ya Kusini Unguja, Singida na Simiyu.

Katika Mkoa wa Kusini Unguja, Kamati imetoa elimu kwa vijana 126 kutoka makundi na madhehebu mbalimbali za dini katika mkutano uliofanyika Septemba 24, 2026 katika ukumbi wa Suni Manzil, pamoja na wanafunzi wa Madrasa ya Kijiji cha Bambi, Shehia ya Mitakawani, wazazi na wajane wa Kijiji cha Mgeni Haji, Wilaya ya Kati. Elimu iliyotolewa ilijikita katika matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano, fursa na changamoto zake, mbinu za kuwatambua matapeli wa mitandaoni na ulazima wa kutoa taarifa Polisi pindi changamoto inapojitokeza.

Mjumbe wa Kamati hiyo, Mohamed Said, alisisitiza kuwa watoto wasio na wazazi ni wahanga zaidi wa matumizi mabaya ya mitandao, hivyo wazazi na walezi wanapaswa kuwa makini na kuwaelimisha mapema.

Hali kadhalika Mkoani Singida, Katibu wa Kamati ya Watumiaji Mkoa wa Singida, Ndg. Rashidi Hamimu, wakati wa mahafali ya wahitimu wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Nkwae, Kata ya Msisi, Wilaya ya Singida Vijijini iliyofanyika Septemba 14, 2026, aliwataka wazazi na walezi kuendelea kuwasimamia na kuwaelekeza vyema watoto kuhusu usalama wao mitandaoni kwa kusisitiza kuwa mzazi au mlezi ndiye mlinzi wa kwanza wa mwanae na anapaswa kusimamia mwongozo wa Ulinzi wa Mtoto Mtandaoni.

Wakati huo huo Mkoani Simiyu, Kamati ya Watumiaji RCC Simiyu imefanikiwa kutoa elimu kwa takribani watu 1,600 katika maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kisomo Duniani yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Wilaya ya Bariadi, ambapo kwa mujibu wa Katibu wa Kamati hiyo, David Wambura, elimu iliyotolewa ilihusu matumizi sahihi ya simu janja, umuhimu wa kusajili laini za simu kwa kutumia kitambulisho halali cha mhusika ili kuepuka changamoto zisizo za lazima, pamoja na namna ya kumlinda mtoto dhidi ya udhalilishaji mtandaoni.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Maafisa Elimu wa Wilaya na Mikoa yote Tanzania, wanafunzi na wadau wa elimu nchi nzima.

Kamati za Watumiaji za Mikoa zina jukumu la kuelimisha, kuhamasisha na kupokea maoni ya watumiaji na kuwasilisha kwa wadau wa sekta wakiwemo watoa huduma za mawasiliano pamoja na Baraza kwa lengo la kupatiwa ufumbuzi.