Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

TCRA Consumer Consultative Council (TCRA-CCC)

Corporate logo

News

​BARAZA LIMEWATAKA WATUMIAJI WA HUDUMA ZA MAWASILIANO KUSHIRIKIANA NA KAMATI ZA WATUMIAJI


BARAZA LIMEWATAKA WATUMIAJI WA HUDUMA ZA MAWASILIANO KUSHIRIKIANA NA KAMATI ZA WATUMIAJI

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA CCC) limewataka watumiaji wa huduma za mawasiliano, kuendelea kutoa ushirikiano kwa Kamati za Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano zilizopo katika Mikoa yao kwa ajili ya kuelimisha, kupokea maoni na kuwasilisha changamoto zinazowakabili kwenye maeneo wanayoishi.

Mary Shao Msuya Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano amesema, Baraza lina Kamati za watumiajikatika Mikoa 18 ya Arusha, Tanga, Iringa, Mbeya, Morogoro, Lindi, Mtwara, Mwanza, Kagera, Dodoma, Kigoma, Pwani, Tabora, Mjini Magharibi, Kusini Pemba, Simiyu, Ruvuma na Rukwa na zimewezeshwa kutekeleza majukumu yao ya kutoa elimu, kuhamasisha na kupokea maoni na changamoto za watumiaji.

“Katika utekelezaji wa majukumu yao Kamati zimeelimisha watumiaji kupitia makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo; watu wenye ulemavu, wanawake, vijana, wajasiriamali, wanafunzi wa shule za Sekondari, viongozi wa dini pamoja na Serikali za mitaa. Masuala yaliyo elimishwa ni pamoja na haki na wajibu wa mtumiaji, fursa na changamoto zilizoko katika sekta, usalama mtandaoni na matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano’’ Amesema Mary Shao Msuya.

Katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2023, Kamati za watumiaji zimewasilisha changamoto mbalimbali ya watumiaji katika Mikoa ambayo ni pamoja na; kutokuwepo bei elekezi ya usafirishaji wa vifurushi, kukatika kwa chaneli za bure ‘Free to Air’ baada ya muda wa malipo ya kifurushi kuisha katika baadhi ya ving’amuzi,changamoto ya mtandao (network) kwenye baadhi ya maeneo pamoja na kupokea ujumbe wa kitapeli.

Aidha; Baraza limejidhatiti katika kushughulikia changamoto husika ikiwemo kuendelea kutoa elimu kwa watumiaji na kuwasilisha kwa watoa huduma changamoto zilizopokelewa kwa lengo la kufanyiwa maboresho ili watumiaji wa huduma za mawasiliano waweze kunufaika na fursa zilizoko katika sekta ya mawasiliano.