News
Serikali Yazindua Kampeni ya Usalama Mtandaoni “SITAPELIKI”
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SERIKALI YAZINDUA KAMPENI YA USALAMA MTANDAONI “SITAPELIKI”
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Jerry William Silaa (Mb), amesema Usalama wa Mitandao ya simu za mkononi na Intaneti utaongeza imani kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano na hivyo kuchagiza shughuli mbalimbali za uchumi wa kidijiti zinazohitaji mitandao salama.
Waziri Silaa ameyasema hayo wakati akizindua Kampeni ya Usalama Mtandaoni yenye jina “SITAPELIKI” wakati wa Kikao Kazi cha Wizara na Wadau wa Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Jengo la PAPU, jijini Arusha.
Aidha, Waziri Silaa aliongeza kuwa uzinduzi huu unalenga kukabiliana na uhalifu kwenye mitandao ya Simu za Mkononi na Intaneti na kuwakumbusha watumiaji wa huduma za mawasiliano kuzingatia tahadhari na elimu inayotolewa kuhusu matumizi sahihi na salama ya mitandao.
Kampeni ya uhamasishaji umma na watumiaji wa huduma za mawasiliano kuhusu njia za kuwa salama mitandaoni na kuepuka ulaghai/utapeli yenye jina la “SITAPELIKI”, inaendeshwa na Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma za Mawasiliano, na wadau wengine.
Amesema kuwa, Ulaghai na hatimaye wizi, hufanyika kwa matapeli kupiga simu kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano na kutuma ujumbe mfupi, na kuwataka watoe taarifa zao zinazohusu akaunti za pesa mtandao, au za kibenki, miamala, nywila (neno la siri).
Utapeli mwingine ni pamoja na ulaghai kwenye mitandao ya kijamii (WhatsApp) kwa kuwashawishi watumiaji kubofya viunganishi (links) vilivyotumwa kama ujumbe au kujibu ujumbe unaohusiana na fursa za kupata pesa za bure, ajira nakadhalika na matokeo yake taarifa za mhusika kudukuliwa na kusababisha matatizo mengine.
Vilevile, Waziri Silaa alisema kuwa Huduma za Mawasiliano nchini zimeenea sana na zinachangia na kurahisisha shughuli mbali mbali za kijamii na za kiuchumi, hivyo Serikali haitavumilia wachache wanaotaka kuleta hofu na kuondoa imani ya matumizi ya huduma za Mawasiliano”.
“Ulaghai mitandaoni unahujumu mikakati ya Serikali kuendeleza ushirikishwaji wa wananchi kwenye mifumo ya kifedha na kujenga uchumi wa kidijiti”, aliongeza. Usalama na uimara wa mitandao unachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa watumiaji wa huduma mbalimbali za mawasiliano zikiwemo huduma za kifedha kupitia simu za mkononi.
Waziri Silaa alitambua mchango wa wadau mbali mbali katika kukabiliana na masuala ya utapeli/ulaghai mtandaoni na kutoa rai kama ifuatavyo:-
- a)TCRA kuendelea kuimarisha usimamizi wa usalama na uimara wa mitandao;
- b)Watoa huduma kutoka katika Makampuni ya simu kuendelea kubuni mbinu mbalimbali za utoaji wa elimu kuhusu usalama mtandaoni na kuwafikia watumiaji wote, pamoja na kuwa na utaratibu maalum wa kushughulikia masuala ya utapeli/ulaghai mtandaoni kwa uharaka pindi wanapopokea malalamiko kutoka kwa wateja.
- c)Vyombo vya Habari kuendelea kushirikiana katika kufikisha ujumbe huu na kuhamasisha jamii yetu kutumia mtandao kwa usahihi na usalama ili waweze kunufaika kikamilifu na fursa zilizopo mtandaoni.
- d)Wadau wengine wote wanaohusika kwa namna moja au nyingine kuhakikisha kuwa wanakuwa mstari wa mbele kushughulikia ipasavyo masuala ya utapeli/ulaghai mtandaoni pindi wanapopokea malalamiko kutoka kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI.
Arusha
21 Februari, 2025