News
Serikali Yazindua Mtumiaji App Kuimarisha Mawasiliano na Kulinda Watumiaji Nchini
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Agellah Jasmine Mbelwa Kairuki, amezindua rasmi mfumo wa kidijitali wa kuhudumia watumiaji wa huduma za mawasiliano ujulikanao kama Mtumiaji App ulioandaliwa na TCRA-CCC, tarehe 23/03/2024 katika ukumbi wa Millennium Towers uliopo jijini Dar es Salaam. Uzinduzi huo umehudhuriwa na wadau wa sekta ya mawasiliano pamoja na wananchi mbalimbali.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Kairuki alisema kuwa uzinduzi wa mfumo huo ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za mawasiliano nchini. Alieleza kuwa mfumo huo utasaidia watumiaji kupata taarifa muhimu, elimu ya matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano pamoja na kutoa nafasi ya kuwasilisha changamoto na maoni yao.
Waziri Kairuki alibainisha kuwa serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali wa mwaka 2024 hadi 2034 uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mkakati huo unalenga kuongeza uelewa wa matumizi ya teknolojia na kuhakikisha wananchi wanatumia mifumo ya kidijitali kwa usalama na ufanisi.
Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), idadi ya laini za simu imeongezeka na kufikia milioni 106.9 hadi Desemba 2025, huku watumiaji wa intaneti wakifikia milioni 58.6. Ongezeko hilo linaonesha kukua kwa kasi kwa sekta ya mawasiliano nchini.
Serikali pia imeendelea kuboresha miundombinu ya mawasiliano kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ambapo jumla ya minara 758 imejengwa na kufikisha huduma katika vijiji zaidi ya 1,400. Hatua hiyo imewezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma za mawasiliano hata katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.
Pamoja na mafanikio hayo, Waziri Kairuki alitaja changamoto zinazokabili sekta hiyo kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa watumiaji, uvunjifu wa faragha, pamoja na vitendo vya utapeli mtandaoni. Alisema mfumo wa Mtumiaji utasaidia kushughulikia changamoto hizo kwa kutoa njia rahisi ya kuwasiliana na wadau husika.


