Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

TCRA Consumer Consultative Council (TCRA-CCC)

Corporate logo

News

TCRA CCC Mkishauri Vizuri Mtaisaidia Serikali


Serikali imelitaka Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA CCC) kuishauri vizuri Serikali ili kupunguza malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za mawasiliano.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi alipotembelea ofisi za Baraza hilo leo Julai 18, 2024 jijini Dar es Salaam.

“Nyie kama wawakilishi wa watumiaji wa huduma kazi yenu kubwa ni kushauri, hivyo mkishauri vizuri mtakuwa mnaisaidia Serikali na kupunguza malalamiko ya wananchi kuhusu huduma zinazotolewa katika sekta ya utangazaji na mawasiliano”, amezungumza Naibu Waziri huyo

Ameongeza kuwa kwa nafasi anayohudumu sasa kama Naibu Waziri wa Wizara hiyo ametembelea Baraza hilo ili kupata uelewa wa majukumu yao lakini pia anatarajia atafanya kazi kwa karibu na Baraza hilo ili kuweza kutoa vizuri majibu ya Serikali kwa waheshimiwa wabunge na kuijibia vema Wizara.

Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji, Mtendaji Mkuu wa TCRA CCC, Bi. Mary Msuya amesema Baraza hilo linawawakilisha watumiaji wa huduma ambazo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inazisimamia kwa kuangalia maslahi ya mtumiaji bila kuumiza upande mwingine.