News
TCRA CCC YAKUTANA NA WATOA HUDUMA ZA MAWASILIANO YA SIMU
Dar es Salaam,
TCRA CCC YAKUTANA NA WATOA HUDUMA ZA MAWASILIANO YA SIMU
Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA CCC) limefanya mkutano na Umoja wa Watoa Huduma za Mawasiliano ya simu (TAMNOA) kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayomhusu mtumiaji wa huduma za mawasiliano ili kuboresha huduma kwa watumiaji, mkutano huo pamoja na mambo mengine umeangazia changamoto za watumiaji na namna ambavyo TCRA CCC, watoa huduma na wadau wengine wanaweza kuzishughulikia ili kuondoa kero kwa watumiaji.
Baadhi ya masuala yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na changamoto ya kutokuwepo kwa internet kwa baadhi ya maeneo na kupelekea muda wa vifurushi kuisha bila kutumika kwa changamoto ambayo haijasababishwa na mtumiaji mwenyewe. Baraza limeshauri watoa huduma kuweka utaratibu wa fidia ya kifurushi kilichoisha bila kutumika kutokana na kutokuwepo huduma husika.
Katika majadiliano hayo imebainika kuwa changamoto ya kutokuwepo kwa mazingira rafiki ya upatikanajiwa huduma kwa watumiaji wenye ulemavu katika Ofisi au maduka ya watoa huduma imekuwa ikiathiri huduma kwa watu wenye ulemavu. Baraza limeshauri watoa huduma kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu kwa kuweka miundombinu rafiki na huduma zitakazohitajika kama vile maeneo ya kutumika na wanaotumia viti mwendo, kuweka wakalimani wa lugha ya alama na huduma zingine wezeshi.
Aidha; Baraza limewasilisha kwa watoa huduma changamoto ya watumiaji kutumiwaujumbe wasioutaka kwenye simu zao, kuhusu masuala kama vile kamari, waganga wa jadi, uponyaji, maombi na maombezi.Baraza limeshauri watumiaji wasitumiwe ujumbe ambao hawajaomba ama kuridhia kama inavyoelekeza kwenye Kanuni za ‘Value Added Services’.
Katika wasilisho lililowasilishwa na Katibu Mtendaji Bi. Mary Shao Msuya imebainishwa kuwa vigezo na masharti ya huduma havifahamiki vizuri na watumiaji na wakati mwingine kuwa katika lugha ya kitaalamu ambayo sio rahisi kueleweka kwa mtumiaji wa kawaida. Katika changamoto hiyo Baraza limeshauri watoa huduma waelimishe kuhusu vigezo na masharti kabla ya watumiaji kuanza kutumia huduma na viwe katika lugha rahisi na yenye kueleweka kwa mtumiaji.
Katika kuhakikisha watanzania wengi wananufaika na ukuaji wa sekta ya mawasiliano Baraza limeshauri watoa huduma kuja na mipango itakayo hamasisha kuhakikisha watumiaji wengi wanakuwa na uwezo wa kumiliki simu janja ili kuweza kunufaika na fursa zilizopo katika sekta. Kutokana na taarifa ya TCRA ya Julai hadi Septemba 2023 simu ndogo (viswaswadu) ziko 51.6 Milioni simu janja ni 18.9 Milioni pekee. Baraza linashauri watoa huduma kuwa na mkakati wa kukomesha simu kwa bei nafuu na mikopo husika iwe rafiki na masharti ambayo watumiaji wa kawaida wataweza kukopa na kulipa taratibu.
Katika mkutano huo watoa huduma walipata fursa ya kutoa ufafanuzi wa masuala yaliyowasilishwa na Baraza. Kupitia utekelezaji wa kazi zake, Baraza litatoa mrejesho kwa watumiaji ili kuongeza uelewa kwa watumiaji na hivyo kupunguza changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza.