Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

TCRA Consumer Consultative Council (TCRA-CCC)

Corporate logo

News

Ubatili wa Mabadiliko ya Bei za Vocha za Simu za Mkononi


Hivi karibuni, kumekuwa na malalamiko ya watumiaji wa huduma za mawasiliano kuhusu kupanda kwa bei za vocha za simu za mkononi katika maeneo mbalimbali. Bei hizo zimekuwa zikitofautiana baina ya wauzaji; hivyo kusababisha malalamiko kutoka kwa watumiaji.

Baraza limepokea taarifa kupitia Kamati za Watumiaji za Mikoa, pamoja na taarifa zilizowasilishwa kwetu na watumiaji zikionyesha kuwa vocha ya shilingi 500 inauzwa kati ya shilingi 550 hadi 600, vivyo hivyo vocha ya shilingi 1,000 kuuzwa kati ya shilingi 1,100, hadi 1,200 kinyume na bei elekezi inayoonyeshwa kwenye vocha husika

Mikoa ambayo Baraza limepokea malalamiko hayo ni pamoja na Dar es Salaam, Rukwa, Iringa, Ruvuma, Manyara, Lindi, Mbeya, Mtwara na Songwe. Baraza linaendelea kufuatilia katika Mikoa mingine kwa lengo la kupata taarifa zaidi juu ya bei za vocha.

Katika kushughulikia changamoto hiyo, Baraza limeshauriana na watoa huduma za Mawasiliano ya simu kufuatilia mawakala wao na kupiga marufuku Upandishaji holela wa bei za vocha.

Aidha; Baraza limeshauri watoa huduma za mawasiliano ya simu kutoa taarifa kwa watumiaji kwa kuwataka kutonunua vocha kwa bei tofauti na inayoonekana kwenye vocha husika na utaratibu wa kutoa malalamiko wanapokutana na kadhia hiyo.

Baraza linashauri watumiaji wa huduma za mawasiliano kununua vocha kwa kupitia simu zao za mkononi wakati changamoto hii ikitafutiwa ufumbuzi na kuendelea kutoa taarifa za kupanda bei kiholela katika maeneo mbalimbali ya nchi ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria na hali hiyo kukomeshwa.

Baraza linaendelea kufuatilia hali hiyo na kushauri hatua za kuchukua ili kuhakikisha watumiaji wa huduma za mawasiliano wanapata haki ya kupata huduma kwa bei halali na yenye ubora.

Imetolewa Tarehe 7 Juni, 2024

__________________

Mary Shao Msuya

KATIBU MTENDAJI