Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

TCRA Consumer Consultative Council (TCRA-CCC)

Corporate logo

News

WANAFUNZI WA CHUO CHA USIMAMIZI WA FEDHA RUKWA WAPATIWA ELIMU JUU YA MATUMIZI SAHIHI YA HUDUMA ZA MAWASILIANO


WANAFUNZI WA CHUO CHA USIMAMIZI WA FEDHA RUKWA WAPATIWA ELIMU JUU YA MATUMIZI SAHIHI YA HUDUMA ZA MAWASILIANO

Kamati ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Mkoa wa Rukwa imetoa elimu kuhusu haki na wajibu wa mtumiaji, pamoja na fursa zilizoko katika sekta ya mawasiliano. Kamati imetoa elimu hiyo katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha kampasi ya Rukwa(Rukwa Institute Business Management) kilichopo katika Manispaa ya Sumbawanga.

Mwenyekiti wa Kamati ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Mkoa wa Rukwa amesema utaratibu huu ni wa kawaida kwa kamati kwakuwa wamejiwekea malengo ya kuwafikia watumiaji maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wanafahamu kuhusu haki na wajibu wao wanapotumia huduma na bidhaa za mawasiliano.

‘’Tumetoa elimu hii kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwakuwa wao ni miongoni mwa watumiaji wengi wa huduma za mawasiliano na ukiangalia kwa makini ndio wanaokabiliana na changamoto mbalimbali watumiapo huduma za mawasiliano hasa mitandao mbalimbali ya kijamii, na tulichogundua ni kwamba bado elimu inahitaji juu ya matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano kwa vijana.’’Alisema Mwenyekiti wa Kamati.

Aidha; amewataka watumiaji wa huduma za mawasiliano Mkoani Rukwa kuendelea kuipa ushirikiano Kamati yao kwa kuwasilisha maoni na changamoto zinazowakabili na amewahakikishia kuwa Kamati inafanya kazi usiku na mchana katika kuendelea kutoa elimu na kuwajengea uwezo watumiaji wa huduma za mawasiliano, lengo likiwa ni kuhakikisha kundi kubwa la wanafunzi wa elimu ya juu wanufaike na fursa zinazopatikana katika matumizi ya huduma za mawasiliano Nchini.