News
Wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Kusini Pemba Wapatiwa Elimu ya Matumizi Sahihi ya Huduma za Mawasiliano
📍Kusini Pemba
Katika jitihada za kukabiliana na utapeli mtandaoni na changamoto mbalimbali za Matumizi ya huduma za mawasiliano nchini, Kamati ya Watumiaji wa Huduma na Bidhaa za Mawasiliano Mkoa wa Kusini Pemba, imetoa elimu kwa wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ili kuwajengea uelewa wa matumizi sahihi na salama ya huduma za mawasiliano.
Aidha; lengo la elimu hiyo ni kuwajengea uwezo watumiaji ili waweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Katibu wa Kamati, Ndugu Khatib Kombo, alieleza watumiaji kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya vifaa vya mawasiliano katika kutokomeza uhalifu mtandaoni, hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano na kuwasaidia watumiaji kuelewa na kutumia vifaa vya mawasiliano kwa usalama zaidi.
Ndugu Kombo amesema "Ni muhimu kuhakikisha kuwa, laini ya simu inapaswa kusajiliwa kwa kitambulisho cha Taifa cha mtumiaji na kuhakikisha kuwa mtumiaji hatoi nywila (password) kwa mtu mwingine yeyote"
Elimu hii ni muhimu katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano hivyo kusaidia kuboresha usalama wa jamii na kuwawezesha kuendana na maendeleo ya teknolojia nchini ikiwemo kutumia fursa zinazopatikana kupitia huduma za mawasiliano ikiwemo biashara mtandao na hivyo kukuza na kuimarisha dhana ya uchumi wa kidijitali.
#KuwaSmart
#HudumaBoraYaMawasilianoNiHakiYako