News
World Consumer Rights Day 2024
Maadhimisho ya Siku ya Haki za Mtumiaji 2024 Kitaifa Kufanyika Jijini Dar Es Salaam
Maadhimisho ya Siku ya Haki ya Mtumiaji Duniani kitaifa mwaka 2024, yatafanyika jijini Dar es Slaam katika ukumbi wa Karimjee, siku ya Ijumaa tarehe 15.03.2024 huku yakiwakutanisha wadau mbalimbali ili kujadili masuala mtambuka yanayowahusu watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa na zisizodhibitiwa hapa nchini.
Mgeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho hayo, yanayobebwa na kaulimbi ya “Fair and Responsible AI for Consumers” anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Albert Chalamila. Katika maadhimisho hayo, Mhe. Chalamila atahutubia makundi mbalimbali ya wadau washirika wa TCF.
“Maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika kwa namna ya mdahalo ambapo wadau mbalimbali kutoka sekta za maji na nishati, mawasiliano, usafiri wa anga na wa nchi-kavu watajadiliana namna teknoljia ya akili bandia inavyoweza kuwaathiri watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa na zisizodhibitiwa hapa nchini,” alisema Daud G. Daud, Mwenyekiti wa Jukwaa la Watumiaji Tanzania (TCF) huku akiongeza kuwa umefika wakati sasa watoa huduma nchini wajikite katika matumizi ya teknolojia ya AI katika kurahisha upatikanaji wa huduma na kutatua changamoto za watumiaji.
Kaulimbiu ya maadhimisho kwa mwaka huu inaenda sambamba na jitihada za Serikali na dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha matumizi ya serikali-mtandao na kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kiteknolojia katika utendaji wa taasisi za umma, ikiwemo teknolojia ya matumizi ya akili bandia (AI) ili kufikisha na kurahisisha huduma kwa watumiaji.
Ikumbukwe kuwa, watumiaji wanaweza kunufaika kwa namna mbalimbali kwa uwepo wa AI kama vile kudhibiti usalama wa ndege kwa usafiri wa anga. Vivyo hivyo, katika usafiri wa nchi kavu, teknolojia ya AI inaweza kutumika katika kuboresha usimamizi wa foleni, kudhibiti usalama barabarani, na kuboresha huduma kwa abiria.
Kwa upande wa matumizi ya huduma za nishati na maji, AI inaweza kutumika kutengeneza mita za kisasa katika kupima matumizi ya wateja, kubaini mivujo ya maji n.k.
Kuhusu mawasiliano, kupitia mifumo ya AI makampuni ya mawasiliano yanaweza kutoa huduma bora zaidi za simu na intaneti kwa kuzingatia mahitaji ya watumiaji, na kuongeza ufanisi wa mitandao.
Kwa muktadha huo, TCF itatumia maadhimisho haya kujadili namna AI inapaswa kuzingatia maslahi na haki za watumiaji. Mdahalo utaongozwa na wataalam wabobevu katika teknolojia ya mawasiliano na usalama, huku ukihusisha wadau wa ndani na nje ya washirika wa TCF. Wanahabari, vyombo vya habari na umma kwa ujumla mnakabishwa tujadili namna AI inaweza kunufaisha watumiaji na utoaji huduma huku ikizingatia haki, wajibu na usalama.
Maadhimisho ya Siku ya Haki za Mtumiaji nchini kwa mwaka huu yameandaliwa na kuratibiwa na Jukwaa la Watumiaji, linaloundwa na Taasisi zinazowatetea watumiaji ambazo ni LATRA CCC, EWURA CCC, TCRA CCC, na TCAA CCC, kwa upande wa Tanzania bara, na kwa upande wa Zanzibar ZFCT na ZFCC.