Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

TCRA Consumer Consultative Council (TCRA-CCC)

Corporate logo

News

PRESS RELEASE


TAARIFA KWA UMMA

UBATILI WA MABADILIKO YA BEI ZA VOCHA ZA SIMU ZA MKONONI

Hivi karibuni, kumekuwa na malalamiko ya watumiaji wa huduma za mawasiliano kuhusu kupanda kwa bei za vocha za simu za mkononi katika maeneo mbalimbali. Bei hizo zimekuwa zikitofautiana baina ya wauzaji; hivyo kusababisha malalamiko kutoka kwa watumiaji.

Taarifa mbalimbali Baraza lilizopata kupitia Kamati za Watumiaji za Mikoa pamoja na taarifa zinazosambaa kupitia vyombo vya habari, zinaonyesha kuwa vocha ya shilingi 500 inauzwa kwa shilingi 550 hadi 600. Vivyo hivyo vocha ya shilingi 1,000 kuuzwa kwa shilingi 1,100 hadi 1,200.

Baraza, kupitia Kamati ya Watumiaji ya Mkoa wa Lindi imebaini uwepo wa hali hiyo katika Wilaya ya Liwale Kata za Mbaya, Mihumo, Likongowele, Kichonda. Maeneo mengine ni Nachingwea kata za Nditi, Mnero, Miembeni, Nambalapala, Kilima Rondo, Lionja na Lindi Manispaa katika Kata za Nangaru, Mtimba, Chikonji, Mipingo, Kitomanga na Kilangala.

Kamati ya Watumiaji ya Mkoa wa Arusha imebaini hali hiyo katika kata ya Sombetini na sehemu nyingine.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano, gharama za vocha za simu hazijapanda. Watumiaji wanapaswa kununua vocha kwa bei husika ambayo inaandikwa katika vocha anayonunua.

Kwa msingi huo muuzaji yeyote anayeuza vocha kwa bei tofauti na iliyoidhinishwa anafanya kosa la Jinai na anapaswa kuripotiwa kituo cha Polisi ili aweze kuchukuliwa hatua.

Baadhi ya watoa huduma wameeleza kwamba wamefanya mabadiliko katika kamisheni wanazopata wasambazaji wakubwa wa huduma za vocha. Baadhi ya wasambazaji wakubwa wameshusha makato ya kamisheni kwa wauzaji wadogo wa rejareja; na wauzaji wa rejareja wameongeza gharama za vocha kwa watumiaji.

Baraza linatamka kwamba mabadiliko yoyote ya kamisheni kwa wauzaji wa jumla hayapaswi kubebeshwa mtumiaji wa mwisho kwani makubaliano ya kamisheni ni kati ya mtoa huduma na mfanyabiashara husika.

Aidha; Baraza linashauri watoa huduma kujadiliana na mawakala wao namna bora ya kutoza kamisheni bila kumuongezea mtumiaji mzigo wa gharama zitokanazo na mabadiliko ya kamisheni, pale yanapokuwepo.

Wakati changamoto hii ikiendelea kupatiwa ufumbuzi Baraza linawashauri watumiaji kununua muda wa maongezi kupitia simu za mkononi.

Katika kuhakikisha kuwa hali hii haiendelei kujitokeza, Baraza linashauri watumiaji wa huduma za mawasiliano kuendelea kutoa taarifa za kupanda bei katika maeneo mbalimbali ya nchi ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria na hali hiyo kukomeshwa.

Baraza litaendelea kufuatilia hali hiyo na kushauri hatua za kuchukua kwa haraka ili kuhakikisha watumiaji wa huduma za mawasiliano wanapata haki ya kupata huduma kwa bei halali na yenye ubora.

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Tanzania limeanzishwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya mwaka 2003 iliyorekebishwa Mwaka 2017 kwa lengo la kuwakilisha maslahi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano kwa kushauriana na Serikali, TCRA na watoa huduma za simu, intaneti, utangazaji na posta.

Huduma Bora za Mawasiliano ni Haki Yako

Imetolewa na:

Katibu Mtendaji

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA CCC)

Dar es Salaam, 10/01/2023.