Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

TCRA Consumer Consultative Council (TCRA-CCC)

Corporate logo

News

REGIONAL CONSUMER COMMITTEES CAPACITY BUILDING MEETING


JESHI la Polisi, Kitengo cha Makosa ya Mtandaoni, limesema wastaafu wanaongoza kwa kutapeliwa mafao yao kwa njia ya uhalifu wa mtandaoni. Kundi lingine ni wanawake wanaoingia kwenye uhusiano na vijana wenye nia ovu na usambazaji wa picha za ngono mtandaoni.

Mchunguzi wa Makosa ya Mitandao, Kisayansi na Upelelezi wa Jeshi la Polisi, Innocent Silvery, aliyasema hayo jana Jijini Dar es Salaam, wakati akizijengea uwezo wa kukabiliana na makosa ya mtandao Kamati za Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano za mikoa kupitia Baraza la ushauri la watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA- CCC). Kamati hizo zilitoka katika mikoa ya Lindi, Pwani, Tanga, Mtwara, Kusini Pemba na Mjini Magharib. Alisema kwa kipindi cha Januari hadi Mei mwaka huu, walipokea kesi 1,239 za matukio ya uhalifu wa mtandaoni na mwaka jana walipokea kesi 2,551.

"Wizi wa makosa ya mtandaoni kwa njia ya hadaa ni tatizo kubwa linaloongoza kwa makosa ya mitandaoni kwa asilimia 90 na kuumiza watu wengi hasa wastaafu kuibiwa mafao yao," alisema Silvery. Alisema wengine wanatapelewa kwa kutaja namba za siri za akaunti ya benki yenye fedha na kukuta fedha zote zimehamishwa.

"Tunapokea kesi nyingi za benki kulalamika wateja wao kuibiwa siyo kwa sababu benki hazipo salama! ila ni kwa sababu wananchi hawana uelewa wa kutunza taarifa zao muhimu za benki. Wastaafu wengi wanaibiwa mafao yao kwa njia hii," alifafanua. Silvery alisema utapeli huo unafanyika kwa kutumia jumbe fupi za maandishi (SMS) kupiga simu, kutuma barua pepe na kukutana ana kwa ana.

Alisema kwa kundi la wanawake wanaokutwa na utapeli wa fedha na mali, wengi wanaanzisha uhusiano na watu wenye nia ovu na mwisho kufanya uhalifu huo. Alisema kuna kundi la wahalifu wanatengeneza picha za ngono na kuanza kuzisambaza na wale ambao wamekuwa wakipiga kutumia simu zao na ikitokea zimepotea wanajikuta mitandaoni na wahalifu hutumia njia hiyo kuomba fedha.

"Wapo wanaotengeneza kwa nia ya kuchafua na kuhitaji fedha kutoka kwa wahusika, wapo wanaozipata picha za watu halisi za utupu na kuzitumia kuwatishia ili kutoa fedha kuzuia zisisambazwe na tatizo hili linawakuta wanawake na mabinti hasa wanafunzi wa vyuo," alisema Silvery na kuongeza kuwa;

"Hakuna faida au maana yoyote kuwa na picha ya uchi kwenye simu, isipokuwa hasara, endapo simu itapotea au mtu kuichukua kwa nia ovu na kujitumia, matokeo yake kuzisambaza mitandao ambako hata Jeshi la Polisi tukichukua hatua itakuwa imeshakuharibia maisha yako yote."

Alisema pia kuna picha za uchi za watoto wa miaka kuanzia saba hadi 10 zinasambazwa mitandaoni na wazazi wanaanza kuombwa hela ili wazifute. Alisema picha hizo zinapatikana kwa njia ya watoto kutumia simu ya mzazi na kuingia kwenye mlangilio ambao sio sahihi na kukutana na mitandao inayoamuru kufanya hivyo bila mzazi kujua.

"Usimpe mtoto simu achezee, wanajua simu kuliko wazazi wenyewe, wakikutana na wahalifu wa mitandaoni wanaambiwa wapige picha wakishapiga wanazituma wewe hujui, siku unaona umetumiwa unaombwa fedha," alisema Silvery. Alisema ukuaji wa teknonojia ni tatizo kubwa linalosababisha kushindwa kuendana na kasi na kuendelea kuongeza kwa uhalifu huo.

Alitaja mikakati ya kukabiliana na tatizo hilo ni kutoa elimu kwa jamii na wana mpango wa kutoa elimu kwa taasisi za elimu ya juu zote nchini.

"Elimu ni chanzo kikubwa cha kuepuka madhara na makosa ya mtandao. Kushirikiana na mashirika ya kikanda na kimataifa tunaendelea kupata elimu ya namna ya kukabiliana nayo lakini pia tunahimiza mlinzi wa kwanza ni muhusika mwenyewe na watu wamekuwa wakiingia kwenye makosa bila kujua,"

Naye Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Bidhaa za Mawasiliano TCRA, Thadayo Ringo, alionya watu wanaosumbuliwa na wahalifu kuacha tabia ya kuwapigia na kuwatukana kwa lengo la kuwakomesha. "Ukishamshtukia mhalifu kama huyo, akikata simu hupaswi kumpigia simu, ukifanya hivyo TCRA hatuwezi kujua mwalifu ni yupi kati yenu, lakini na yeye anaweza kukuripoti kuwa ni mwalifu na ukafungiwa laini yako," alionya.