Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

TCRA Consumer Consultative Council (TCRA-CCC)

Corporate logo

News

WANUFAIKA WA KAYA MASIKINI WAPEWA SOMO KUEPUKA UTAPELI KWA NJIA YA MTANDAO


WANUFAIKA WA KAYA MASIKINI WAPEWA SOMO KUEPUKA UTAPELI KWA NJIA YA MTANDAO

Kamati ya watumiaji wa huduma za mawasiliano Mkoa wa Kusini Pemba wametekeleza dhima ya kutoa elimu kwa watumiaji kwa kuwafikia moja kwa moja wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini.

Khatib Bakari Kombo Katibu wa Kamati ya watumiaji wa huduma za mawasiliano Mkoa wa Kusini Pemba amesema utaratibu wa kutoa elimu kwa mtumiaji ni majukumu ya kamati hiyo ya kila siku kwa kuwa wamekuwa wakitoa elimu kuhusiana na haki na wajibu wa mtumiaji, lakini pia wamekuwa wakitoa elimu kuhusiana na umuhimu wa matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano Nchini.

Kombo amesema kuwa wameona kuna umuhimu mkubwa wa kufikisha elimu ya watumiaji kupitia wananchi walio katika kaya maskini wakati wanapatiwa ruzuku katika shehia ya matale kwakuwa kuna changamoto nyingi zinazowakabili hususani kuwepo kwa utapeli kwa njia ya mtandao na wengine kudhulumiwa pesa zao zote za ruzuku.

Aidha Katibu huyo wa Kamati ya watumiaji Mkoa wa Kusini Pemba ameongeza kwa kusema kuwa kumekuwa na changamoto ya uelewa juu ya kukabiliana na utapeli kwa njia ya mtandao unaofanywa na baadhi ya watu ambao sio waaminifu kwa wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini hasa kwenye kipindi ambacho wanapatiwa ruzuku hivyo wameona ni vyema kuwapatia elimu jinsi ya kukabiliana na utapeli kwa njia ya mtandao na kuongeza kuwa mpango huo ni endelevu wakiwa wamepanga kugusa jamii yote kwa ujumla.

Naye Bi.Fatuma Mohamed Juma mnufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini ameshukuru kwa elimu waliyopatiwa kuhusiana na matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano. Lakini pia wametambua umuhimu wa kufahamu haki na wajibu wao wakiwa wanatumia huduma za mawasiliano na ameongeza kuwa wamekuwa wakikabiliwa na tatizo kubwa la utapeli kwa njia ya mitandao hasa kipindi hiki ambacho wamepokea ruzuku kwani elimu hii waliyopatiwa imewasaidia kutambua mbinu za utapeli kwa njia ya mitandao.

Aidha ameshukuru kupatiwa elimu ya kufahamu umuhimu wa Kusajili line za simu kupitia wao binafsi na kutokutimia line zilizosajiliwa na watu wengine na wameomba elimu hiyo iwe endelevu.

Kamati za Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano zimeanzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano ya Mwaka 2003, Kifungu cha 38.Lengo likiwa ni kuhamasisha watumiaji wa huduma na bidhaa za Mawasiliano Nchini kutambua haki na wajibu wao,pamoja na kukusanya maoni na kero za watumiaji na kuziwasilisha kwa Baraza.